Kushambuliwa kambi ya wakimbizi Darfur Sudan
Watu wenye silaha wameishambulia kambi ya wakimbizi katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan na kuua watu wasiopungua watatu na kuwajeruhi wengine 11.
Chini ya wiki mbili zilizopita pia, watu wenye silaha walifanya shambulizi kama hilo kusini mwa jimbo hilo na kujeruhi watu sita. Shambulio katika kambi ya wakimbizi huko Darfur limefanyika katika hali ambayo maelfu ya wakazi wa jimbo hilo wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia mapigano baina ya wanajeshi wa serikali na waasi, hata hivyo inaonekana kuwa wakazi wa jimbo hilo hawana usalama hata katika kambi za wakimbizi. Serikali ya Sudan imetoa muda wa miezi mitatu wa kukabidhi silaha kwa hiari. Viongozi wa Khartoum wamesema kuwa, baada ya kumalizika muda huo, mtu yeyote atakayemiliki silaha kinyume cha sheria atahesabiwa kuwa ni muhalifu. Kura ya maoni kuhusu imma kuunganishwa na kuwa moja jimbo la Darfur au kuendelea kuwa katika majimbo matano tofauti ni mpango mwingine uliopendekezwa na serikali ya Sudan, kama njia ya kudhibiti hali ya mambo kwenye eneo hilo. Kura hiyo ya maoni ilifanyika tarehe 13 hadi 15 mwezi uliopita wa Aprili. Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa na serikali, karibu asilimia 98 ya walioshiriki kwenye kura hiyo waliunga mkono kuendelea kuweko majimbo matano tofauti katika eneo hilo. Matokeo hayo yameifurahisha serikali ya Khartoum kwani inaifungulia njia ya kulidhibiti zaidi eneo hilo. Hata hivyo makundi mawili makuu ya waasi wa Darfur yaani kundi la Uadilifu na Usawa na lile la Jeshi la Ukombozi wa Sudan, yameituhumu serikali ya Khartoum kuwa inawachezea shere wananchi. Kufanyika kura ya maoni ya kuamua hatima ya majimbo matano ya eneo lililokumbwa na machafuko la Darfur, ndiyo matakwa makuu ya waasi kwa muda mrefu. Hata hivyo wapinzani wa serikali ya Sudan wanasema kuwa, mazingira ya kuitisha kura hiyo hayapo hivi sasa. Wanasema, matokeo ya kura hiyo ya maoni hayawezi kubainisha matakwa halisi ya wananchi wa Darfur. Sababu inayotolewa na wapinzani hao ni kuwa wananchi wengi wa eneo hilo wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na machafuko. Hivi sasa hali imezidi kuwa mbaya katika eneo hilo, suala ambalo linazidi kutilia nguvu madai ya wapinzani. Inavyoonekana ni kuwa, amani katika jimbo la Darfur itaweza kupatikana pale tu zitakapojadiliwa sababu hasa wa kuweko machafuko hayo na kuandaliwa mazingira mazuri ya kufanyika kura huru ya maoni itakayoyashirishika makundi yote ya Darfur, sambamba na kufanyika mazungumzo baina ya Wasudan wote kuhusu suala hilo. Wapinzani wanaamini kuwa, kufanyika kura ya maoni katika wakati huu ambapo serikali inadhibiti maeneo mengi ya Darfur ni katika njama tu za serikali za kukabiliana na matakwa ya waasi ya kulifanya eneo la Darfur kuwa eneo moja tu. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, ni jambo lililo mbali kuweza kupatikana utulivu wa kudumu huko Darfur kutokana na hali ilivyo hivi sasa, na kwamba kura hiyo ya maoni haiwezi kuwadhaminia wakazi wa eneo hilo usalama wao. Kuvamiwa na kushambuliwa kambi ya wakimbizi katika eneo hilo hivi karibuni, ni uthibitisho wa uhakika huo.