Magaidi 76 wa al-Shabaab wauawa na jeshi la Somalia
(last modified Sun, 04 Apr 2021 11:02:21 GMT )
Apr 04, 2021 11:02 UTC
  • Magaidi 76 wa al-Shabaab wauawa na jeshi la Somalia

Jeshi la Somalia limesema kuwa limeangamiza makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika operesheni ya kiusalama kusini mwa Somalia.

Brigedia Jenerali Mohamed Tahlil Bihi, Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Nchi Kavu cha Somalia amesema wanachama 76 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab waliuawa mapema jana katika operesheni ya kuzuia hujuma za wanamgambo hao dhidi ya kambi mbili za kijeshi katika wilaya za Awdhigle na Bariire katika eneo la Lower Shabelle, kusini mwa Somalia.

Brigedia Jenerali Bihi ameongeza kuwa, wanachama wengine kumi wa kundi hilo la kigaidi walitiwa mbaroni katika operesheni hiyo ya alfajiri ya jana Jumamosi.

Mashuhuda wanasema miili ya wanamgambo wa al-Shabaab imetapakaa katika maeneo yalipojiri makabiliano ya mtutu wa bunduki baina ya magaidi hao na wanajeshi wa Somalia.

Wanajeshi wa Somalia wakielekea katika operesheni ya kiusalama

Hapo jana, Jeshi la Taifa la Somalia lilitangaza kuwa, askari wa nchi hiyo wamefanikiwa kuzima mashambulio ya kundi la kigaidi la al-Shabaab yaliyolenga kambi hizo mbili za kijeshi kusini mwa nchi.

Hata hivyo genge hilo la ukufurishaji kupitia msemaji wake, Abdiasis Abu Musab lilidai kuwa limeua 'wanajeshi kadhaa' katika mashambulio hayo, yapata kilomita 100 kusini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu, mbali na eti kuharibu magari ya deraya na zana za kivita za jeshi la Somalia.

Tags