Nigeria yatuma makumi ya askari polisi wake nchini Somalia
Kikosi cha askari polisi 144 wa Nigeria kimewasili nchini Somalia, kwenda kupiga jeki jitihada za kurejesha uthabiti katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Daniel Ali Gwambal, Mratibu wa Operesheni za Polisi za Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM amesema maafisa hao wa polisi kutoka Nigeria waliwasili nchini Somalia jana Jumapili.
Amesema 30 miongoni mwao watahudumu chini ya mwavuli wa AMISOM kwa muda wa mwaka mmoja katika mji wa Beletweyne jimboni HirShabelle na waliosalia watapewa majukumu tofauti katika mji mkuu, Mogadishu.
AMISOM imesema kuwasili kwa maafisa hao wa polisi kutokana Nigeria kutatoa mchango mkubwa katika jitihada za kudhamini na kuimarisha usalama hususan katika maeneo ambayo yamekombolewa toka mikononi mwa magenge ya kigaidi.
Maelfu ya wanajeshi wa AMISOM walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na Sierra Leone, huku maafisa wa polisi wa kikosi hicho cha Umoja wa Afrika wakitokea Nigeria, Sierra Leone na Uganda.
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM wanaokadiriwa kufikia 21,000 wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 ili kujaribu kukabiliana na magaidi wa al-Shabab.
Hata hivyo pamoja na jitihada hizo za kimataifa, magaidi wa al-Shabab wanaendelea kutekeleza hujuma Somalia na katika nchi jirani ya Kenya.