Tanzania, Kenya zaafikiana kuhusu ujenzi wa bomba la gesi
(last modified Tue, 04 May 2021 15:00:47 GMT )
May 04, 2021 15:00 UTC
  • Rais Uhuru Kenyatta (kulia) na Rais Samia Suluhu Hassan
    Rais Uhuru Kenyatta (kulia) na Rais Samia Suluhu Hassan

Kenya na Tanzania zimefikiana kuhusu ujenzi wa bomba la gesi aina ya LPG kutoka Dar es Salaam kwenda Mombasa.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo Jumanne jijini Nairobi nchini Kenya baada ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwasili nchini humo kwa ziara ya siku mbili kufuatia mwaliko rasmi Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi habari akiwa ameandamana na Rais Suluhu, Rais Kenyatta amesema: "Tumekubaliana kwamba na tumeweka mkataba, wa kujenga bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, hiyo itarahisisha bei ya stima na kusaidia, viwanda vyetu kupata nishati safi.”

Kwa ujumla, leo Tanzania na Kenya zimekubaliana mambo matano kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa nchi hzi mbili.

Alipowasili mapema leo mjini Nairobi, Rais Samia Suluhu Hassan amekaribishwa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi na kisha alikagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga 21.

Rais Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride la heshima katika Ikulu ya Rais mjini Nairobi

 Rais Samia amesema Kenya ni mdau mkubwa wa biashara na uwekezaji. Akifafanua kuhusu nukta hiyo, amesema, "Wakati wa mazungumzo yetu nimemwarifu Kenyatta kuwa Kenya inashika nafasi ya tano kwa uwekezaji nchini kiulimwengu, lakini katika nchi za Afrika Mashariki inashika nafasi ya kwanza.” Amesema Kenya imewekeza miradi 513 yenye thamani ya Dola 1.7 bilioni ambayo imetoa ajira 51,000 za Watanzania.  Aidha amesema zipo kampuni 30 za Tanzania zimewekeza mtaji ndani ya Kenya na kutoa ajira kwa watu 2,640 hivi.

Rais Kenyatta amesema kuwa wamekubaliana kuwa Tume ya Pamoja ya mawaziri wa nchi hizo mbili iwe inakutana mara kwa mara ili kutatua changamoto za kibiashara na uhusiano zinatazotokea.

Rais Samia Suluhu Hassan anazuru Kenya takribani mwezi mmoja na nusu baada ya kuchukua hatamu za uongozi nchini Tanzania. Ziara yake ya pili nje ya Tanzania baada ya kuzuru Uganda majuma matatu yaliyopita.