Mshukiwa wa Sudan anayesakwa kwa jinai za Darfur afadhilisha ICC
Afisa wa zamani wa serikali ya Sudan anayetuhumiwa kuhusika na jinai zilizofanyika katika eneo la Darfur amesema anafadhilisha kufikishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC badala ya faili lake kusikilizwa nchini Sudan.
Ahmed Haroun amekuwa akisakwa na ICC kwa zaidi ya muongo mmoja sasa akiandamwa na mashitaka ya jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita zilizofanyika wakati wa mgogoro wa Darfur, uliozuka mwaka 2003. Malaki ya watu wasio na hatia waliuawa katika mapigano hayo katika eneo la Darfur.
Haroun pamoja na shakhsia wengine kadhaa wa utawala uliopita wa Sudan wanaotuhumiwa kuhusika na jinai hizo za Darfur walitiwa mbaroni nchini Sudan baada ya kujiri tukio la kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al-Bashir Aprili mwaka 2019.
Siku ya Jumatatu, Haroun alifikishwa mbele ya kamati ya uchunguzi nchini Sudan inayofuatilia jinai zilizofanyika katika mapigano hayo ya Darfur.

Katika taarifa yake yenye kurasa tano ya Mei 3, mshukiwa huyu anadai kuwa maafisa wa serikali ya sasa ya Sudan wanamzulia kwa 'nia mbaya' kinyume cha sheria, na kwamba Mkuu wa Mashitaka amemnyima haki yake ya kupinga mashitaka dhidi yake.
Taarifa hiyo iliyosambaa jana Jumanne katika mitandao ya kijamii imeeleza kuwa: Utawala huu wenye utendaji mbovu wa masuala ya sheria hauwezi kutenda haki na kwa msingi huu, natangaza kwa yakini kuwa nafadhilisha kesi dhidi yangu, iwapo zipo, ziwasilishwe katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.