Wanamgambo 10 wa ADF waangamizwa na jeshi la Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i69990-wanamgambo_10_wa_adf_waangamizwa_na_jeshi_la_kongo_dr
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza habari ya kuwauwa wanamgambo wasiopungua 10 wa ADF mashariki mwa nchi, katika operesheni dhidi ya genge hilo la wapiganaji.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2021 22:21 UTC
  • Wanamgambo 10 wa ADF waangamizwa na jeshi la Kongo DR

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza habari ya kuwauwa wanamgambo wasiopungua 10 wa ADF mashariki mwa nchi, katika operesheni dhidi ya genge hilo la wapiganaji.

Msemaji wa Jeshi la DRC, Antony Mualushayi amesema wanamgambo hao wameuawa katika kijiji cha Halungupa eneo la Rwenzori, katika operesheni ya kiusalama iliyoanza tokea Alkhamisi iliyopita.

Ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, idadi hiyo ya wanamgambo wa ADF walioangamizwa ni ya muda, kwani operesheni hiyo inayokusudia kulisambaratisha kikaimilifu kundi hilo katika mikoa miwili ya mashariki mwa nchi inaendelea.

Siku chache zilizopita, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitangaza 'hali ya mzingiro' katika mikoa miwili ya  Ituri na Kivu Kaskazini inayoshuhudia mapigano na umwagaji damu kwa miezi kadhaa sasa.

Wanamgambo wa ADF

Ongezeko la mashambulizi ya magenge yenye silaha na machafuko ya kikabila yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 300 tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, huku wanajeshi wa serikali na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakijaribu kuleta utulivu mashariki mwa nchi hiyo bila mafanikio.

Kundi la ADF ambalo asili yake ni Uganda na ambalo linasemekana kuwa na mfungamano na genge la kigaidi la ISIS (Daesh) limeua raia zaidi ya 1,000 tokea Novemba mwaka 2019 katika mji wa Beni pekee, mashariki mwa Kongo DR.