Waziri Mkuu wa Sudan alaani mauaji ya maandamano mjini Khartoum
(last modified Thu, 13 May 2021 07:07:21 GMT )
May 13, 2021 07:07 UTC
  • Waziri Mkuu wa Sudan alaani mauaji ya maandamano mjini Khartoum

Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok amesema "ameshtushwa" na mauaji ya waandamanaji wanaotetea haki za Wasudani waliouawa na askari usalama miaka miwili iliyopita na ameyataja mauaji ya sasa kuwa ni "uhalifu wa kutumia risasi hai dhidi ya watu wanaoandamana kwa amani".

Kwa uchache watu wawili wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa wakati askari usalama wa Sudan walipokabiliana na maandamano ya raia wanaodai haki za waandamanaji wenzao waliouawa wakati wa maandamano dhidi ya serikali ya Khartoum miaka miwili iliyopita.

Mamia ya Wasudani walikusanyika Jumanne jioni nje ya makao makuu ya jeshi katika mji mkuu, Khartoum, eneo ambako maelfu ya raia walikusanyika mwaka 2019 wakitaka kuondolewa madarakani rais wa wakati huo, Omar al-Bashir na kuundwa utawala mpya wa kiraia.

Maandamano hayo ya Jumanne yalianza muda mfupi kabla ya iftar, chakula cha jioni ambacho huliwa na Waislamu kufungua swaumu wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Jeshi la Sudan limetangaza kuwa, limeanzisha uchunguzi wa kubaini wahusika wa mauaji hayo.

Taarifa ya jeshi la Sudan imesema, Jeshi liko tayari kabisa kumfikishwa mahakamani yeyote atakayethibitishwa kuhusika.

Waandamanaji mjini Khartoum

Katika maandamano hayo, waandamanaji walionekana wakiwa wamebeba mabango na picha za watu waliouawa wakati wa ukandamizaji wa 2019.

Waandamanaji hao wamesema wataendeleza maandamano hadi pale serikali itakapotangaza matokeo ya uchunguzi wake kuhusu mauaji ya mwaka 2019.

Watu wasiopungua 128 waliuawa kwa kupigwa risasi katika maandamano ya raia wa Sudan yaliyopelekea kuondolewa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir.

Al Bashir alioongoza Sudan kwa kipindi cha miongo mitatu.

Tags