Watu 50 wauawa katika shambulio la ADF mkoani Ituri, DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i70768-watu_50_wauawa_katika_shambulio_la_adf_mkoani_ituri_drc
Kwa akali watu 50 wameuawa katika shambulio la kundi la wanamgambo wa ADF dhidi ya vijiji viwili mashariki mwa mkoa wa Ituri huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
May 31, 2021 22:45 UTC
  • Watu 50 wauawa katika shambulio la ADF mkoani Ituri, DRC

Kwa akali watu 50 wameuawa katika shambulio la kundi la wanamgambo wa ADF dhidi ya vijiji viwili mashariki mwa mkoa wa Ituri huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Msemaji wa jeshi la DRC, Jules Ngongo ameliambia shirika la habari la DPA kuwa, watu wasiopungua 53 wameuawa katika hujuma ya usiku wa kuamkia jana ya genge la ADF lenye mfungamano na kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) dhidi ya vijiji vya Boga na Tchabi katika mkoa wa Ituri, mashariki mwa nchi.

Mbunge wa eneo hilo, Gracien Iracan amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa, wanavijiji waliouawa katika shambulio hilo la magaidi wa ADF ni zaidi ya 60.

Amesema yumkini idadi hiyo ikaongezeka kwa kuwa miili inaendelea kupatikana katika vijiji husika, huku idadi kubwa ya waliojeruhiwa wakiwa bado wamejificha katika misitu ya karibu. Vijiji hivyo vipo katika mpaka wa mikoa wa Ituri na Kivu Kaskazini, maeneo ambayo wanachama wa ADF wanaendesha sana harakati zao.

Ramani ya DRC inayoonesha mkoa wa Ituri

Baadhi ya maafisa wa serikali katika vijiji hivyo hata hivyo wametadharisha dhidi ya kulilaumu genge la ADF kwa mauaji hayo, wakisisitiza kuwa yumkini mauaji hayo yametokana na mapigano ya kikabila.

Ongezeko la mashambulizi ya magenge yenye silaha na machafuko ya kikabila yamesababisha vifo vya mamia ya watu tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, huku wanajeshi wa serikali na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakijaribu kuleta utulivu mashariki mwa nchi hiyo bila mafanikio.