Rais Samia awatahadharisha Watanzania dhidi ya Corona
Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania waendelee kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Rais Samia alitoa mwito huo jana Jumanne, Juni Mosi, alipofanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali Rufaa ya Mkoa Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Amesema baadhi Watanzania wanaziba midomo kwa kutumia barakoa na vifaa vingine lakini wengine hawafanyi hivyo, hali inayowaweka kwenye hatari kubwa hivyo ni vema kila mmoja akafanya jitihada za kujikinga.
Mama Samia ameeleza bayanakuwa, “Sasa hivi tuko vizuri, lakini mnasikia wenzetu huko India mambo yanavyowapukutisha watu wamechoma hadi kuni hamna kwahiyo desturi ya mambo haya yanaambukiza na yakitoka sehemu moja yanaenda sehemu nyingine."
Amebainisha kuwa, “Tumejitahidi kuzuia usafiri wa kutoka kule kuja huku au hapa kwenda kule ili virusi visije, kwahiyo kila mtu achukue tahadhari pale alipo, kama ni kunawa mikono na kwa bahati mbaya anayekuja nacho humjui,”amesema.
Rais wa Tanzania ameongeza kkuwa, “Tumepokea vya aina yote sijui cha South Afrika, sijui vya wapi sasa hivi kuna vya India, kila mtu achukue tahadhari pale alipo kama ni kunawa mikono kujikinga ili tuepukane na lile balaa kubwa.”