UNHCR: Volkano ya Nyiragongo imevuruga maisha ya wengi DRC
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR na wadau wengine wanaendelea kutoa msaada kwa watu waliolazimika kuyakimibia makazi yao baada ya mlipuko wa volkano katika Mlima Nyiragongo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.
Kwa mujibu wa UNCR, volcano hiyo imevuruga maisha ya watu wengi ambao walivuka mpaka kwenda nchi jirani ya Rwanda ambako sasa wanapata usaidizi.
Baada ya kuingia Rwanda, wakimbizi hawa walisajiliwa ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR pamoja na wadau wanawapatia pia msaada wa chakula na malazi.
Wakimbizi waliozungunza na waandishi habari wanasema waliona mlipuko wa moto kutoka volkano ya Nyiragongo na kisha matope ya moto au lava kutoka mlima huo yakatiririka na kuua watu na pia kuharibu mashamba pamoja na nyumba na vijiji.
Wakazi wengi wa eneo hilo walikimbilia nchi jirani ya Rwanda ili kuokoa maisha yao
Mara ya mwisho Mlima Nyiragongo kumwaga volkano yake ilikuwa mwaka 2002 ambapo watu zaidi ya 200 waliaga dunia na wengine 100,000 walipoteza makazi yao.
UNHCR inasema mlipuko wa mwaka huu ambao ulianza Mei 22 umesababisha vifo vya watu 32, na wengine 350,000 wanahitaij msaada. Mlipuko huo umesita kwa sasa lakini wakazi wa eneo hilo bado wana wasiwasi kuwa yamkini ukatokea tena hivi karibuni na hivyo wengi wamechukua tahadhari na hawajarejea makwao.
Volkano ya Mlima Nyiragongo inatajwa kuwa miongoni mwa volkano hai na hatari duniani.