Makumi ya watoto nchini Cameroon waokolewa kutoka mikononi mwa Boko Haram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7093-makumi_ya_watoto_nchini_cameroon_waokolewa_kutoka_mikononi_mwa_boko_haram
Serikali ya Cameroon imetangaza kuwa, imewakomboa makumi ya wanawake na watoto waliokuwa wakishikiliwa na kundi la kigaidi la Boko Haram.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 15, 2016 04:13 UTC
  • Makumi ya watoto nchini Cameroon waokolewa kutoka mikononi mwa Boko Haram

Serikali ya Cameroon imetangaza kuwa, imewakomboa makumi ya wanawake na watoto waliokuwa wakishikiliwa na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Msemaji wa serikali ya Cameroon amesema kuwa, vikosi vya mataifa kadhaa vinavyoshiriki operesheni dhidi ya Boko Haram mwanzoni mwa mwezi huu vilishambulia ngome kadhaa za Boko Haram kaskazini mwa nchi hiyo na kufanikiwa kuwakomboa kwa uchache watoto 28 na wanawake 8.

Issa Tchiroma Bakary amebainisha kuwa, wanachama watano waandamizi wa kundi hilo la Boko Haram walitiwa mbaroni katika operesheni hiyo.

hayo yanajiri katika hali ambayo, mkutano wa usalama wenye lengo la kujadili mbinu na mikakati ya kupambana na kundi la Boko Haram ulianza jana katika mji mkuu wa Nigeria Abuja.

Kundi la Boko Haram lililoanzisha machafuko ya ndani nchini Nigeria mwaka 2009 limeua zaidi ya watu elfu 20 na kulazimisha mamilioni ya wengine kukimbia maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo. Mbali na Nigeria wanamgambo hao sasa wanaendesha harakati zao za kigaidi katika nchi za Chad, Niger, Cameroon na hata Benin.