Jeshi la Somalia laangamiza magaidi 130 wa al-Shabaab
(last modified Tue, 08 Jun 2021 02:50:12 GMT )
Jun 08, 2021 02:50 UTC
  • Jeshi la Somalia laangamiza magaidi 130 wa al-Shabaab

Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) limetangaza habari ya kufanikiwa kuua wanachama wasiopungua 130 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.

SNA ilitangaza hayo jana Jumatatu na kueleza kuwa, magaidi hao wameuawa katika operesheni zilizoongozwa na kamanda mwandamizi wa jeshi hilo, Brigedia Jenerali Odowaa Yusuf Rage katika eneo la Shabelle ya Kati. 

Taarifa ya Jeshi la Taifa la Somalia imeongeza kuwa, operesheni ya kusafisha mabaki ya genge hilo lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda katika eneo la Shabelle ya Kati inaendelea. 

Silaha na zana za kijeshi zilizokuwa zikitumiwa na magaidi hao wakufurishaji zimenaswa pia katika operesheni hiyo.

Jumanne iliyopita, wanamgambo wasiopungua 30 wa al-Shabaab waliangamizwa katika operesheni ya wanajeshi wa serikali ya Somalia katika eneo la Hiran, katikati mwa nchi.

kamanda mwandamizi wa jeshi hilo, Brigedia Jenerali Odowaa Yusuf Rage

Kabla ya hapo pia, Jeshi la Somalia lilitangaza kuwa wanamgambo wengine 100 wa genge hilo la kigaidi wakiwemo makamanda wake kadhaa wameangamizwa katika operesheni nyingine maalumu ya kijeshi huko kusini mwa Somalia.

Genge la al-Shabaab lilianzishwa nchini Somalia mwaka 2004 na tangu wakati huo hadi hivi sasa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika haijawahi kuwa na utulivu wa angalau siku moja, licha ya operesheni za wanajeshi wa nchi hiyo wakishirikiana na askari wa kulnda amani wa Umoja wa Afrika (AMISOM).

Tags