Jeshi la Somalia laendelea kutoa kipigo kwa magaidi wa al-Shabaab
Kundi la kigaidi la al-Shabaab limeendelea kuandamwa na wimbi la vipigo kutoka kwa Jeshi la Taifa la Somalia (SNA), ambalo linatazamiwa kutwikwa jukumu la ulinzi na usalama wa nchi baada ya kumalizika muda wa Mpango wa Mpito wa Somalia (STP).
Magaidi 17 wa genge hilo la ukufurishaji wameangamizwa katika operesheni nyingine ya kuwatokomeza wanachama wa kundi hilo katika eneo la Hiraan, katikati mwa Somalia.
Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, magaidi hao waliangamizwa jana Ijumaa, baada ya wanajeshi wa Somalia kufanya shambulio la kushtukiza dhidi ya maficho ya kundi hilo katika wilaya ya Mahaas.
Haya yanajiri siku chache baada ya wanamgambo 60 wa genge hilo la kigaidi kuangamizwa katika mripuko wa bomu uliotokea kwenye kijiji kimoja kilichoko umbali wa takriban kilomita 65 Magharibi mwa Qoryooley huko Kusini mwa Somalia.
Jeshi la Somalia limezidisha operesheni zake katika majimbo ya katikati na Kusini mwa nchi hiyo hadi magaidi wote wanaoua raia na watu wasio na hatia watakaposafishwa kikamilifu kwenye maeneo hayo.
Jumatatu iliyopita, Jeshi la Somalia lilitangaza habari ya kufanikiwa kuua wanachama zaidi ya 150 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika kipindi cha wiki tatu, katika operesheni zinazoongozwa na kamanda mwandamizi wa jeshi hilo, Brigedia Jenerali Odowaa Yusuf Rage katika eneo la Shabelle ya Kati.