Afrika Kusini: Watu wasiopungua 45 wameuawa katika maandamano ya kumuunga mkono Zuma
Idadi ya waliofariki dunia kutokana na vurugu na uporaji unaoendelea Afrika Kusini kwa siku kadhaa sasa imeongezeka hadi 45.
Vifo 22 vimetangazwa mapema leo Jumanne na Waziri Mkuu wa mkoa wa KwaZulu Natal Mashariki, Sihle Zikalala na hivyo kuifanya idadi watu walioaga dunia katika jimbo hilo ambako ghasia zilianza Ijumaa iliyopita, kufikia 26.
Sihle Zikalala ameongeza kuwa, watu sita wameaga dunia katika jiji la Johannesburg, kama ilivyothibitishwa na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini Jumatatu ya jana.
Jeshi la Afrika Kusini liliitwa jana Jumatatu ili kudhibiti vurugu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Ghasia na maandamano hayo yaliyoanzia katika mkoa wa KwaZulu Natal baada ya mwanasiasa huyo kufungwa jela kwa tuhuma za kuhusika na ufisadi, zimeathiri mji wa Johannesburg ambao ndio makao makuu ya kichumi ya Afrika Kusini.
Katika ghasia za jana Jumapili, waandamanaji walishambulia na kupora maduka huku wakifunga barabara kuu za mji huo.
Wiki iliyopita Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini iliagiza Zuma afungwe jela kwa kukataa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa ufisadi uliofanyika katika kipindi chake cha uongozi kutoka 2009 hadi 2018.
Rais mstaafu wa Afrika kusini Jacob Zuma, alijikabidhi kwa polisi siku kadhaa zilizopita na kupelekwa katika gereza lililo karibu na nyumbani kwake katika jimbo la KwaZulu Natal.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametoa wito kwa Waafrika Kusini kuzingatia athari mbaya vitendo vyao na machafuko ya sasa nchini humo.
Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini alilazimika kujiuzulu mwezi Februari mwaka 2018 kutokana na mashinikizo ya chama tawala cha ANC kwa tuhuma za kuhusika na ufisadi na utumiaji mbaya wa madaraka yake.