Mafuriko yasababisha maafa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i72456-mafuriko_yasababisha_maafa_jamhuri_ya_kidemokrasia_ya_congo
Mafuriko yaliyotokea kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 16.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 17, 2021 07:52 UTC
  • Mafuriko yasababisha maafa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Mafuriko yaliyotokea kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 16.

Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA imesema kuwa, mvua kubwa zilizonyesha kuanzia mwezi Machi hadi Mei 2021 huko kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimesababisha mito kujaa maji, kufurika na kuvunja kingo za mito hiyo.

Watu zaidi ya 16 wamepoteza maisha, zaidi ya nyumba 26 elfu zimeharibiwa na maji na zaidi ya shule 260 na vituo vya matibabu katika mkoa wa Tanganyika, vimesababishiwa hasara kubwa na mafuriko hayo.

 

Ripoti mpya ya OCHA inaonesha kuwa, watu laki mbili na 80,000 wameathiriwa vibaya na mafuriko huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na mvua hizo kubwa zilizosababisha hasara za roho na mali.

Takriban mwaka mmoja nyuma pia, watu wasiopungua 40 walifariki dunia kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na watu 75,000 walipoteza makazi yao.

Mafuriko na maporomoko ya udongo hutokea kila mwaka huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Matukio hayo mara nyingi huanzia mwezi wa Aprili na nyumba nyingi hukombwa na mafuriko, kuharibiwa, roho za watu hupotea kutokana na mvua kali za masika.