13 wapoteza maisha Kenya baada la lori la petroli kulipuka
Watu 13 wamepoteza maisha na wengine kadhaa wamejeruhiwa wakati lori la mafuta lilipoanguka na kuripuka, magharibi mwa Kenya.
Taarifa zinasema watu hao walifariki wakati walipokuwa wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika kutoka kwenye lori hilo. Tukio hilo lilijiri jana usiku majira ya saa tatu.
Ajali hiyo imeripotiwa kutokea wakati dereva alipojaribu kupishana na lori lingine katika barabara ya Kisumu na Busia.
Watu hao walikimbilia eneo la tukio kuchota mafuta wakati lori hilo lilipopinduka lakini ghafla likawaka moto.Watu wapatao 11 wakiwemo watoto, wapo hospitalini wakiwa na hali mbaya baada ya kuungua.
Charles Chacha mkuu wa polisi katika mji wa Siaya, amesema watu 12 walikufa katika eneo la tukio na mmoja alifariki hospitalini kutokana na majeraha mabaya ya moto aliyoyapata. Watu wengine wengi wakiwemo watoto wanaendelea kupata matibabu hospitalini.

Chacha amesema lori lililokuwa limebeba maziwa kutoka Busia, kariu na mpaka wa Uganda kuelekea Kisumu liligongana na lori hilo la mafuta lililokuwa linaelekea eneo tofauti.
Mwaka 2009 kisa kama hicho kilichotokea Molo kaskazini magharibi mwa Nairobi kilisababisha vifo vya watu 122.