Iran: Tunafuatilia kwa karibu matukio yanayojiri Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i72840-iran_tunafuatilia_kwa_karibu_matukio_yanayojiri_tunisia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inafuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa yanayoendelea kushuhudiwa hivi sasa nchini Tunisia.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jul 27, 2021 20:59 UTC
  • Iran: Tunafuatilia kwa karibu matukio yanayojiri Tunisia

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inafuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa yanayoendelea kushuhudiwa hivi sasa nchini Tunisia.

Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana Jumanne na kuongeza kuwa, Iran imesimama bega kwa bega na Tunisia na inatumai kuwa nchi hiyo itavuka salama kipindi hiki cha sasa.

Ametoa mwito kwa pande zote husika nchini humo kuwa na umoja na kusisitiza kuwa, mazungumzo ndiyo njia pekee ya kuliondoa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika katika mtihani wa sasa.

Khatibzadeh amegusia kuhusu umuhimu wa usalama na uthabiti wa kisiasa katika nchi hiyo ya Kiarabu na kueleza kuwa, anatumai kuwa wananchi wa Tunisia watavuka kipindi hiki hasasi haraka iwezekanavyo kupitia njia ya mazungumzo.

Wananchi wa Tunisia wamekuwa wakiandamana kwa muda sasa kulalamikia ughali wa maisha

Taharuki ingali imetanda katika maeneo mbali mbali ya nchi, kufuatia uamuzi wa Rais wa nchi hiyo, Kais Saeid kuwafuta kazi Waziri Mkuu na Spika wa Bunge, sambamba na kusimamisha shughuli za Bunge la nchi hiyo.

Rached Ghannouchi, Spika wa Bunge la Tunisia amekosoa uamuzi uliochukuliwa na Rais Kais Saeid akisema hatua iliyochukuliwa na rais ya kusitisha shughuli za Bunge na kumfuta kazi Waziri Mkuu Hichem Mechichi ni jaribio la mapinduzi dhidi ya mapinduzi, katiba na uhuru wa Tunisia.