Rais wa Tunisia ampiga kalamu nyekundu Balozi wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73158-rais_wa_tunisia_ampiga_kalamu_nyekundu_balozi_wa_marekani
Katika kile kinachoonekana ni kushtadi mgogoro wa kisiasa nchini Tunisia, Rais Kais Saied wa nchi hiyo ametangaza kumfuta kazi Balozi wa nchi hiyo huko Marekani pamoja na Gavana wa moja ya mikoa ya kistratajia ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 04, 2021 22:03 UTC
  • Rais wa Tunisia ampiga kalamu nyekundu Balozi wa Marekani

Katika kile kinachoonekana ni kushtadi mgogoro wa kisiasa nchini Tunisia, Rais Kais Saied wa nchi hiyo ametangaza kumfuta kazi Balozi wa nchi hiyo huko Marekani pamoja na Gavana wa moja ya mikoa ya kistratajia ya nchi hiyo.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo vimesema Rais Saeid amemtimua kazi Nejmeddine Lakhal, Balozi wa Tunisia nchini Marekani pasi na kutoa maelezo yoyote ya kina. Katika dikrii hiyo mpya, Rais wa Tunisia amemfuta kazi pia Anis Oueslati, Gavana wa mkoa muhimu wa Sfax, ulioko mashariki mwa nchi.

Haya yanajiri siku moja baada ya rais huyo kuendeleza timua timua yake kwa kumfukuza kazi Ali Kooli, Waziri wa Uchumi pamoja na Waziri wa Mawasiliano wa nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Wiki iliyopita, Rais huyo wa Tunisia mwenye umri wa miaka 63, alitoa amri ya kufukuzwa kazi orodha ndefu ya maafisa wakuu wa serikali, pamoja na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Jeshi.

Bunge la Tunisia

Tarehe 25 mwezi Julai mwaka huu, Rais Kais Saeid wa Tunisia alimfuta kazi Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Hicham Mechichi na kisha akasimamisha shughuli za Bunge akisema amechukua hatua hiyo katika juhudi za kurejesha amani na uthabiti nchini humo.

Wapinzani wake wameitafsiri hatua hiyo kuwa ni mapinduzi baridi aliyofanya kwa kushirikiana na jeshi la nchi hiyo. Spika wa Bunge la Tunisia lililosimamishwa, Rached Ghannouchi amesema hatua aliyochukua Rais Kais Saied ni mapinduzi dhidi ya mapinduzi ya wananchi, katiba ya nchi na uhuru wa taifa.