Makamu wa Rais wa Sudan Kusini atoswa na chama chake
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini ameenguliwa kuwa kiongozi wa chama chake na vile vile mkuu wa vikosi vya jeshi alivyokuwa akiviongoza.
Chama cha upinzani cha SPLM-IO ambacho kimegawana madaraka na chama cha SPLM kinachoongozwa na Rais Salva Kiir kimemtosa Machar, licha ya kiongozi huyo kuwa na mchango mkubwa katika kufikiwa mapatano ya amani ya 2018.
Tawi la kijeshi la chama hicho alichokuwa anakiongoza Machar SPLM/A-IO limesema Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini ametimuliwa uongozini baada ya kufanyika mkutano wa siku tatu huko kaskazini mwa nchi hiyo.
Taarifa ya Tawi la kijeshi la chama cha SPLM-IO imeeleza bayana kuwa, Mkuu wa vikosi hivyo, Luteni Jenerali Simon Gatwech Dual, ndiye ameteuliwa kuwa kaimu kiongozi wa harakati hiyo ya upinzani.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Machar ameshindwa kabisa kuonesha uongozi imara, na badala yake amekidhoofisha zaidi chama hicho cha upinzani na nafsi yake ndani ya serikali ya muungano iliyoundwa mapema mwaka 2020.
Nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ilitumbukia kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu makamu wake wakati huo, Machar kuwa alipanga njama ya kumpindua.