Waalgeria: ISIS ni genge lililoundwa na Marekani
Wananchi wengi wa Algeria wanaamini kuwa, genge la kigaidi la Daesh (ISIS) limeundwa na Marekani.
Gazeti la Fajr la Algeria lilitangaza jana (Jumatano) kuwa, kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi moja ya Ujerumaini huko Algeria, wananchi wengi wa nchi hiyo wanaamini kuwa, Daesh ni genge lililoundwa na Marekani. Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni, karibu asilimia 50 ya wananchi wa Algeria wanaamini kuwa, chanzo cha misimamo mikali ya kidini ni nchi za Magharibi na si ulimwengu wa Kiislamu. Mchunguzi mmoja wa taasisi hiyo ya Kijerumani anayejulikana kwa jina la Konrad Adenauer amefanya uchunguzi kuhusu uhusiano baina ya wananchi wa Algeria na dini na kusema kuwa, karibu asilimia 99.8 ya wananchi wa Algeria wanaamini kuwa, kuweko dini ya Kiislamu katika maisha yao ya kila siku ni jambo lenye umuhimu mkubwa sana. Uchunguzi huo aidha umeonesha kuwa, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Algeria wanaamini kuwa utambulisho wao wa kidini ni bora zaidi kuliko utambulisho wao wa kitaifa. Uchunguzi huo wa hatua na maudhui mbalimbali umefanyika kwenye miji mikubwa na pia katika vijiji vya ndani kabisa vya Algeria na unaonesha pia kuwa, asilimia kubwa sana ya wananchi wa Algeria wanaona kwamba, kuweko misikiti katika maeneo yao ni neema kubwa. Ikumbukwe kuwa zaidi ya asilimia 99 ya wananchi wa Algeria ni Waislamu na asilimia iliyobakia ni ya watu wa dini nyingine kama vile Wakristo na Mayahudi.