Watu kadhaa wauawa na waasi wa ADF mjini Beni, Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73422-watu_kadhaa_wauawa_na_waasi_wa_adf_mjini_beni_kongo_dr
Watu wasiopungua watatu wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika shambulizi la waasi wa kundi la ADF katika eneo la Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 12, 2021 03:38 UTC
  • Watu kadhaa wauawa na waasi wa ADF mjini Beni, Kongo DR

Watu wasiopungua watatu wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika shambulizi la waasi wa kundi la ADF katika eneo la Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Afisa wa serikali katika eneo hilo amesema raia hao waliuawa jana Jumatano, baada ya wapiganaji wa ADF waliojizatiti kwa silaha kushambulia kijiji cha Kainama katika eneo la Beni.

Isaya Muhindo amesema waasi hao walivamia kijiji hicho Jumanne, lakini milio ya risasi ilikuwa inasikika hadi jana nyakati za adhuhuri. Amesema watu hao waliuawa baada ya kutoka katika maeneo walikojificha, baada ya kusikia milio ya risasi imenyamaza.

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeripotiwa kuanzisha operesheni ya kuwafurusha na kuwarejesha nyuma wapiganaji hao wa kundi la kigaidi la ADF.

Wanamgambo wa ADF

Mwishoni mwa mwezi uliopita, jeshi la DRC lilitangaza kuwa, limefanikiwa kuwaokoa raia zaidi 150 waliokuwa wametekwa na kundi hilo la waasi huko mashariki mwa nchi hiyo.

Ongezeko la mashambulizi ya magenge yenye silaha hususan waasi wa ADF-NALU wa Uganda wanaoendesha harakati zao mashariki mwa DRC; na machafuko ya kikabila yamesababisha vifo vya mamia ya watu tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.

Hii ni katika hali ambayo, wanajeshi wa serikali na walinda amani wa Umoja wa Mataifa wamejaribu kuleta utulivu mashariki mwa nchi hiyo ya katikati mwa Afrika bila mafanikio.