Boti iliyobeba makumi ya wahajiri yatoweka baharini pwani ya Mauritania
Watu 47 wakiwemo watoto wadogo watatu wanahofiwa kupoteza maisha baada ya boti iliyokuwa imewabeba kupoteza mkondo na kutoweka, baada ya injini yake kufeli katika pwani ya Mauritania.
Gadi ya Pwani ya Mauritania imewanukuu manusura saba wa ajali hiyo wakisema kuwa, boti hiyo iliyokuwa imebeba wahajiri 54, ilipoteza mkondo baada ya injini kuharibika, muda mfupi baada ya kuondoka mjini Laayoune eneo la Sahara Magharibi.
Boubacar Seybou, Msemaji wa Shirika la Uhajiri la Umoja wa Mataifa (IOM) amesema, wapiga mbizi wao kwa kushirikiana na mamlaka za Mauritania wanasaka miili ya wahajiri hao, waliokuwa na azma ya kuelekea Kisiwa cha Canary nchini Uhispania.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali ya Uhispania, wahajiri 7,531 kutoka Magharibi mwa Afrika wamewasili katika kisiwa hicho kati ya Januari Mosi na Julai 31, hilo likiwa ni ongezeko la 136%, ikilinganishwa na wakati kama huo mwaka 2020.

Katika wiki za hivi karibuni, wapiga mbizi na timu za waokoaji wameopoa makumi ya maiti za wahajiri waliozama baharini wakiwa katika safari hatarishi za kuelekea Ulaya.
Aghalabu ya wahajiri hao haramu ambao kutokana na sababu za kiuchumi na usalama huamua kuziacha nchi zao kwa tamaa ya kwenda kutafuta kazi na maisha mazuri barani Ulaya, wanatokea katika nchi za Nigeria, Eritrea, Somalia, Sudan, Gambia, Senegal, Mali, Morocco na Tunisia.