Tanzania yaithibitishia WHO kuwa mgonjwa mmoja wa Marburg amegunduliwa nchini humo
Mtu mmoja ambaye alikuwa akiugua ugonjwa wa Marburg amegunduliwa nchini Tanzania.
Hayo yamethibitishwa na Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan katika mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Amesema, serikiali yake ilichukua hatua kufuatia uvumi uliokuwa ukiendelea mkoani Kagera na kwamba sampuli zilizochukuliwa katika hospitali moja mkoani humo na kuthibitishwa mjini Dar es Salaam zilimtambua mtu huyo aliyekuwa na virusi vya maradhi hayo.
Hata hivyo sampuli za washukiwa wengine wa maradhi hayo hazikupatikana na ugonjwa huo hatari.
Rais Samia amebainisha kuwa, hii ni mara ya pili kwa virusi vya maradhi hayo kugunduliwa nchini Tanzania, ambapo mara ya kwanza viligunduliwa mwezi Machi 2023 katika eneo hilohilo la Kagera wilayani Bukoba.
Ameongeza kuwa, kufikia sasa kumekuwepo na visa 25 vya washukiwa wa maradhi ya Marburg ambapo sampuli zao zimepatikana hazina ugonjwa huo lakini serikali inawafuatilia watu hao kwa karibu.
Rais wa Tanzania amelishukuru pia shirika la WHO kwa kuchukua hatua za dharura, akisema serikali yake itachukua hatua kama zile zilizochukuliwa mwaka 2023 kudhibiti maradhi hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ametoa ufadhili wa dola milioni tatu kwa Tanzania ili kusaidia kudhibiti maradhi hayo, ikiwa ni pamoja na dola 50,000 ambazo shirika hilo lilitoa kwa nchi hiyo kusaidia katika uchunguzi.../