Rais wa Tanzania: Uchaguzi wa 2020 ulifanyika vizuri sana tena kwa kiwango kikubwa sana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73770
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kusimamia uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2020 akisema "ulifanyika vizuri sana tena kwa kiwango kikubwa sana."
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 21, 2021 14:01 UTC
  • Rais wa Tanzania: Uchaguzi wa 2020 ulifanyika vizuri sana tena kwa kiwango kikubwa sana

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kusimamia uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2020 akisema "ulifanyika vizuri sana tena kwa kiwango kikubwa sana."

Rais Samia ameyasema hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akipokea ripoti ya uchaguzi mkuu wa madiwani, ubunge na urais uliofanyika Jumatano ya tarehe 28 Oktoba 2020.

Rais wa Tanzania aidha amewapongeza wananchi kwa kushiriki kikamilifu kuanzia zoezi la uandikishaji, kupiga kura na kushiriki uchaguzi mkuu huo ambao chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM) kilitangazwa na NEC kuwa mshindi wa urais na kuzoa karibu majimbo na kata zote.

"Hakuna shaka, yeyote aliyeshuhudia uchaguzi mkuu wa mwaka jana alishuhudia jinsi ulivyofanyika vizuri sana tena kwa kiwango kikubwa sana", amesema Rais Samia.

Hata hivyo amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika uchaguzi huo kuna changamoto pia na kwamba hiyo ndiyo sababu ya kuandaliwa ripoti ili kutoa fursa kwa wadau kuichambua na kutoa mapendekezo ili kuboresha chaguzi zijazo.

Kiongozi huyo amesema, "tuombe uchaguzi ujao uwe bora na mzuri zaidi kulingana na mapendekezo ya tume."

Hayati Magufuli na Samia

Katika uchaguzi mkuu wa rais wa 2020 Rais Samia alikuwa mgombea mwenza wa Dk John Pombe Magufuli aliyetangazwa mshindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Magufuli aliapishwa tarehe 5 Novemba 2020 na Samia akawa makamu wa rais kumaliza ngwe ya miaka mitano. Hata hivyo Magufuli alifariki dunia Machi 17 2021 na Samia akaapishwa kuwa rais wa Tanzania.

Hafla ya leo ya makabidhiano ya ripoti ya uchaguzi mkuu wa 2020 imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wawakilishi wa jumuiya za kimataifa na baadhi ya vyama vya siasa huku vyama vinne vikuu vya upinzani vikisusia shughuli hiyo.

Vyama hivyo vyenye nguvu vilivyosusia ni Chadema, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi na CUF vikidai kwamba kilichofanyika 2020 ni uchafuzi na si uchaguzi huru na wa haki.../