UN yasema malaki wameathiriwa na mafuriko nchini Sudan Kusini
(last modified Wed, 01 Sep 2021 08:00:16 GMT )
Sep 01, 2021 08:00 UTC
  • UN yasema malaki wameathiriwa na mafuriko nchini Sudan Kusini

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imesema watu zaidi ya 380,000 wameathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha nchini Sudan Kusini.

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na OCHA imesema, asilimia 75 ya watu walioathiriwa na mafuriko hayo ambayo yamepelekea mito kuvunja kingo zake, ni wakazi wa majimbo mawili ya Unity na Jonglei.

OCHA imeeleza kuwa, barabara za majimbo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo hazipitiki, huku ikionya kuwa, mvua na mafuriko zaidi yanatazamiwa kushuhudiwa nchini humo katika miezi ijayo.

Muathiriwa mmoja wa mafuriko hayo Michael Gai ambaye amekimbilia mjini Bor, makao makuu ya Jonglei amesema idadi kubwa ya watu katika jimbo hilo wameshindwa kugura kwenda kwenye maeneo salama.

Hadi sasa hakujatolewa idadi ya watu waliofariki dunia na hasara kamili iliyosababishwa na mafuriko hayo katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika. 

Athari za mafuriki Sudan Kusini

Mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana zilivunja rekodi nchini Sudan Kusini, huku mafuriko na maporomoko ya udongo yakiwaathiri watu zaidi ya 700,000.

Katika nchi jirani pia, mafuriko makubwa yaliyosabishwa na mvua kubwa iliyonyesha nchini Sudan yameathiri na kubomoa maelfu ya nyumba za raia hususan huko Khartoum mji mkuu wa nchi hiyo.