Wakenya wapewa matumaini ya kupungua bei ya mafuta na ughali wa maisha
(last modified Sun, 03 Oct 2021 14:52:09 GMT )
Oct 03, 2021 14:52 UTC
  • Wakenya wapewa matumaini ya kupungua bei ya mafuta na ughali wa maisha

Wananchi wa Kenya wamepata matumaini ya kupungua bei ya mafuta nchini humo ambayo imekuwa mzigo kwa raia baada ya Mamlaka ya Kusimamia Kawi na Petroli Nchini (EPRA) kupandisha bei ya bidhaa hiyo.

Bidhaa za mafuta nchini Kenya zinauzwa kwa gharama ya juu ambayo Wakenya hawajawahi kushuhudia.

Afueni hiyo imepatikana baada ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga kudokeza kuwa serikali inatazamiwa kupunguza bei ya mafuta wiki ijayo.

Akizungumza katika kaunti ya Bungoma siku ya Jumamosi, Raila alisema hatua hiyo ni ya kuwalinda Wakenya ambao wameathirika pakubwa na ugumu wa uchumi uliosababishwa na janga la COVID-19.

"Ninawahakikishia kuwa bei ya mafuta itashuka wiki ijayo", amesema Raila Odinga.

Matamashi ya Raila yanakuja baada ya Mamlaka ya Kusimamia Kawi na Petroli Nchini Kenya (EPRA) kupandisha bei ya bidhaa za mafuta mnamo Septemba 14. EPRA ilishtumiwa vikali baada ya kutangaza kuwa bei ya mafuta itapanda. Hatua hiyo ya EPRA ilipelekea kupanda bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kushuhudiwa nchini humo.

Wanasiasa wengi wa Kenya waliguswa pia na suala hilo wakiiomba serikali kuingilia kati na kutafuta suluhu mwafaka.

Suala hilo pia limefikishwa bungeni na wabunge wengi wanaonekana kukubaliana na hoja ya kupunguza bei ya mafuta japokuwa wao ndio waliopitisha muswada wa kuongeza bei ya bidhaa hiyo kwa asiliimia 8.