Baghaei: Machi 19 ni uthibitisho wa dhamira ya Wairani ya kupinga uonevu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa tarehe 29 Isfand (Machi 19), ambayo ni maadhimisho ya siku ya kufanywa mafuta ya Iran kuwa ni mali ya taifa, ni ushahidi wa azma ya kweli ya wananchi wa Iran ya kupinga uonevu.
"Esmail Baghaei" ameandika hayo kwenye mtandao wa kijamii wa X kama sehemu ya kumbukumbu ya kufanywa mafuta ya Iran kuwa mali ya taifa na kuongeza kwamba: "Machi 19 si siku ya kumbukumbu tu kwenye kalenda ya Iran, bali ni ushahidi wa nia ya kweli ya wananchi wa Iran ya kupinga uonevu na vitisho na ni ishara ya utashi wa kitaifa wa kujiamulia wenyewe mambo yao na kulinda heshima yao kitaifa..."
Jana Jumatano ilisadifiana na tarehe 29 Isfand kwa kalenda ya Iran ya Hijria Shamsia yaani (Machi 19, 2025). Siku hiyo huadhimishwa kitaifa hapa Iran kama siku ya kukumbuka mwaka wananchi wa Iran walipofanikiwa kuitoa sekta ya mafuta kwenye makucha ya wakoloni na kuifanya kuwa ni mali ya taifa.
Mpango wa kuyafanya mafuta kuwa ni mali ya taifa uliidhinishwa na Bunge la Iran tarehe 20 Machi, 1951, na tangu wakati huo hadi hivi sasa, utajiri wa mafuta wa Iran unatambuliwa rasmi kuwa ni mali ya wananchi na dola lolote la kigeni halina haki ya kuigusa rasilimali hiyo bila ya idhini ya wananchi wa Iran.