Kesi za Corona barani Afrika zapungua kwa asilimia 13
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i75502-kesi_za_corona_barani_afrika_zapungua_kwa_asilimia_13
Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) kimesema bara la Afrika limeshuhudia kupungua kwa maambukizo ya ugonjwa wa COVID-19 katika kipindi cha wiki moja.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 08, 2021 00:49 UTC
  • Kesi za Corona barani Afrika zapungua kwa asilimia 13

Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) kimesema bara la Afrika limeshuhudia kupungua kwa maambukizo ya ugonjwa wa COVID-19 katika kipindi cha wiki moja.

Mkurugenzi wa Africa CDC, John Nkengasong alisema hayo jana Alkhamisi na kufafanua kuwa, kesi 67,000 za ugonjwa wa COVID-19 zimenakiliwa katika nchi za Afrika kati ya Septemba 27 na Oktoba 3, huko kukiwa ni kupungua kwa asilimia 13 ikilinganishwa na wiki ya kabla.

Amesema katika kipindi hicho cha juma moja, vifo vya maradhi hayo vilivyonakiliwa barani Afrika ni 2,500, ikimaanisha kuwa vimepungua pia kwa asilimia tano.

Afisa huyo wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) amesisitiza kuwa, takwimu hizo zinazoashiria kupungua kwa maambukizi na vifo vya Corona barani Afrika zinatia moyo.

Kwa mujibu wa takwimu za kituo hicho, bara la Afrika kufikia sasa limerekodi zaidi ya kesi milioni 8.4 za ugonjwa huo hatarishi wa kuambukiza, mbali na vifo zaidi ya laki mbili na 13 elfu vya maradhi hayo. Afrika CDC imesema, hadi sasa waliopona baada ya kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19 barani Afrika ni zaidi ya milioni 7.7.

Usafi; moja ya njia nyepesi za kupambana na maambukizi ya Corona

Afrika CDC imesema, ni asilimia 4.5 tu ya watu wa Afrika waliopata chanjo kamili ya Corona kufikia sasa. Bara hilo limepokea dozi milioni 200 za kukabiliana na maradhi ya COVID-19 mpaka sasa, ambapo asilimia 76.77 ya chanjo hizo zimeshatolewa kwa wahitaji.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza hivi karibuni kuwa, nchi 14 za Afrika pekee ndizo zilizokuwa zimetoa chanjo ya Corona kwa zaidi ya asilimia 10 ya jamii zao hadi kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita wa Septemba.