Kenya na Marekani zajadili namna ya kukomesha machafuko Sudan na Ethiopia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Uhuru wa Kenyatta wa Kenya kujadili namna ya kuhitimisha machafuko katika nchi za Sudan na Ethiopia.
Katika mazungumzo yao hayo yaliyofanyika jijini Nairobi rais wa Kenya na waziri wa mambo ya nje wa Marekani wamechunguza fursa mpya za ushirikiano kwa ajili ya kutatua machafuko ya kikanda na kuhakikisha amani endelevu inapatikana katika eneo la Pembe ya Afrika.
Imeelezwa kuwa, katika mazungumo hayo, Kenyatta na Blinken wamezungumzia pia masuala mengine kadhaa likiwemo janga la dunia nzima la ugonjwa wa Covid-19 na mabadiliko ya tabianchi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani pamoja na ujumbe alioandamana nao wamekutana na kufanya mazungumzo pia na waziri wa mambo ya nje wa Kenya Raychelle Omamo.
Baada ya mazungumzo yao, Blinken na Omamo wametangaza kuwa, nchi hizo mbili zimeahidi kushirikiana kwa karibu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kupitia asasi zingine za kikanda na za pande kadhaa kwa ajili ya kuchunguza vyanzo vya kuvurugika uthabiti wa kieneo katika Pembe ya Afrika na maeneo mengine.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Afrika wamekuwa kila mara wakipinga kuwepo kijeshi Marekani katika nchi zao na kusisitiza kuwa ,kuwepo kwa vikosi vya jeshi la Marekani kunashadidisha mapigano na kukosekana amani katika nchi za bara hilo.../