Upinzani kushiriki duru mpya ya mazungumzo ya amani ya Burundi
(last modified Wed, 25 May 2016 04:07:17 GMT )
May 25, 2016 04:07 UTC
  • Upinzani kushiriki duru mpya ya mazungumzo ya amani ya Burundi

Muungano mkuu wa upinzani nchini Burundi unaoitwa CNARED umesema uko tayari kushiriki duru mpya ya mazungumzo ya amani iwapo utaalikwa rasmi.

Pancrace Cimpaye, Msemaji wa muungano huo unaovileta pamoja vyama kadhaa vya upinzani pamoja na wakuu wa zamani wa serikali amesema wako tayari kushiriki mazungumzo yajayo ya kuutafutia ufumbuzi mzozo wa kisiasa nchini Burundi na kusisitiza kuwa mazungumzo yaliyoanza Jumamosi mjini Arusha nchini Tanzania na kumalizika jana, ni ya upande mmoja na hayatakuwa na tija. Amesema duru mpya ya mazungumzo yanafaa kuvileta pamoja vyama vyote vya siasa vikiwemo vya upinzani, mashirika ya kiraia na asasi za kijamii zinazopinga muhula wa tatu kwa Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo.

Benjamin William Mkapa, rais wa zamani wa Tanzania na mpatanishi wa jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki anayesimamia mazungumzo hayo, jana Jumanne katika siku ya mwisho ya vikao hivyo alisema kuwa mazungumzo hayo yamefanyika katika ngazi za kidiplomasia, wawakilishi wa serikali, wajumbe wa chama tawala nchini Burundi CNDD-FDD na kadhalika wawakilishi wa jumuiya za kiraia ndani ya nchi hiyo, na kwamba wanashauriana na viongozi wa kisiasa ambao hawakuhudhuria kikao cha Arusha, kuwashawishi washiriki duru ijayo ya mazungumzo.

Machafuko nchini Burundi yaliibuka mwezi Aprili mwaka jana, baada ya chama tawala kuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kugombea kwa mara ya tatu mfululizo kwenye uchaguzi mkuu uliopita.