5 wauawa katika shambulio la bomu la al-Shabaab kusini mwa Somalia
Watu wasiopungua watano wameuawa katika mripuko wa bomu uliotokea katika mgahawa mmoja wenye shughuli nyingi kusini mwa Somalia.
Omar Mahamed, afisa wa polisi jijini Baidoa, amesema mripuko huo wa bomu ulitokea jana Jumapili katika mji wa Awdhegle, umbali wa kilomita 30 kutoka Baidoa. Baidoa ndio mji mkubwa zaidi katika jimbo la Kusini Magharibi nchini Somalia, yapata kilomita 243 kusini magharibi mwa Mogadishu.
Amesema watu watano akiwemo askari mmoja wa jeshi la Somalia wameuawa katika shambulio hilo la bomu lilioongozwa kutoka mbali. Mashuhuda wameliambia shirika la habari la Anadolu kuwa, watu kadhaa wamejeruhiwa pia kwenye shambulio hilo, akiwemo mwanamke mmoja.
Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limetangaza kuhusika na hujuma hiyo, likidai kuwa shambulio hilo lililenga askari wa jimbo la Kusini Magharibi, na kwamba wanajeshi wawili wameuawa.
Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya wanachama wa genge hilo kushambulia uwanja wa ndege na kambi ya kijeshi ya askari wa Ethiopia katika mji wa Baidoa, ulioko kusini magharibi mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, ambapo askari mmoja na raia mmoja waliuawa.
Hilo lilikuwa shambulio la pili la genge la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda jijini Baidoa, tangu uchaguzi wa Bunge katika eneo hilo uanze siku chache zilizopita.