Mafuriko yaikumba Sudan Kusini
Mvua kubwa zilizonyesha huko Sudan Kusini zimesababisha mafuriko nchini humo.
Takribani asilimia 70 ya jamii ya watu wa Sudan Kusini wameathiriwa na mafuriko hayo kufuatia mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni, huku watu 850,000 pia wakiwa katika hatari ya kuwa wakimbizi.
Beny Makon Naibu Mkuu wa kambi ya wakimbizi katika mji wa Bentiu kaskazini mwa Sudan Kusini amesema kuwa idadi ya watu wanaokabiliwa na tisho kubwa linalotokana na mafuriko baada ya mvua za karibuni kuu imeongezeka.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini ambaye amefanya safari nchini humo kwa lengo la kutathmini maafa na hasara zilizosababishwa na mafuriko ameeleza kuwa, kiwango cha maji yaliyosababishwa na mafuriko kimeongezeka na imeelezwa kuwa uvukizi wake wa kimaumbile utachukua miaka 15.
Njaa na ukame ulioikumba Sudan Kusini pia vimeathiri maisha ya asilimia 60 ya jamii ya nchi hiyo. Sudan Kusini kwa mwaka inahitaji tani milioni 1.3 za chakula na sehemu kubwa ya mahitaji hayo ya chakula hudhaminiwa na taasisi mbalimbali za masuala ya kibinadamu. Mazao mbalimbali ya kilimo yameharibiwa kufuatia mafuriko hayo huko Sudan Kusini.