Wanamgambo 100 wa ISIS wauawa katika mashambulizi ya anga kaskazini mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78332
Shirika la habari la Ufaransa limenukuu vyanzo vya kijeshi na vya ndani vikisema kuwa wapiganaji 100 wa kundi la kigaidi la ISIS waliuawa wiki iliyopita katika mashambulizi ya jeshi la Nigeria dhidi ya kambi za kundi hilo kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 22, 2021 13:37 UTC
  • Wanamgambo 100 wa ISIS wauawa katika mashambulizi ya anga kaskazini mwa Nigeria

Shirika la habari la Ufaransa limenukuu vyanzo vya kijeshi na vya ndani vikisema kuwa wapiganaji 100 wa kundi la kigaidi la ISIS waliuawa wiki iliyopita katika mashambulizi ya jeshi la Nigeria dhidi ya kambi za kundi hilo kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Vyanzo hivyo vimeeleza kuwa Disemba 13, ndege za kivita za jeshi la Nigeria zilishambulia kambi 3 za Daesh (ISIS) katika Jimbo la Afrika Magharibi (ISWAP), na kuua wapiganaji zaidi ya 100 wakiwemo viongozi kadhaa wa kundi hilo.

Kundi hilo la ISIS Jimbo la Afrika Magharibi (ISWAP) lilikuwa limeimarisha udhibiti wake kaskazini mashariki mwa Nigeria tangu kuuawa kwa kiongozi wa Boko Haram, Abubakar Shekau, katika mapigano yaliyojiri kati ya makundi hayo mawili hasimu mwezi Mei mwaka jana.

Kundi la ISWAP lilianzishwa mwaka 2016 baada ya wapiganaji kadhaa wa Boko Haram kujitenga na kundi hilo ambalo wanalishutumu kuwa linaua raia Waislamu.

Afisa mmoja wa jeshi la Nigeria amesema: "Operesheni za anga zilizofanywa na ndege mpya ya Super Tucano katika maeneo ya Arena Soro, Arena Seki and Arena Mamasalachi katika mkoa wa Marti karibu na Ziwa Chad zimeua magaidi zaidi ya 100."

Wanamgambo wa ISWAP

 

Kati ya mwezi Juni na Oktoba mwaka jana Nigeria ilipokea takriban ndege 10 za kivita za Super Tucano kwa ajili ya kupambana na makundi ya kigaidi.

Chanzo kimoja cha kilicho karibu na shirika la ujasusi la Nigeria kimeeleza kuwa ni vigumu kutoa idadi maalumu ya wapiganaji waliouawa katika operesheni hizo, lakini kimethibitisha kuwa idadi hiyo ni zaidi ya 100.

Idadi kubwa ya wanamgambo wa ISWAP walikimbilia hifadhi katika maeneo hayo  matatu baada ya jeshi la Nigeria kushambulia kwa mabomu miji kadhaa inayodhibitiwa na kundi hilo siku chache zilizopita.

Wavuvi wa eneo hilo wamethibitisha kwamba kundi hilo lilipata hasara kubwa wakati wa mashambulio hayo ya jeshi la Nigeria na kwamba limezika zaidi ya miili 100 na lilihitajia siku nzima kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo."