Indhari kuhusu kurejea udikteta huko Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78624-indhari_kuhusu_kurejea_udikteta_huko_tunisia
Rached Ghannouchi Spika wa Bunge lililosimamishwa la Tunisia amezitaja hatua na maamuzi yanayochukuliwa na Rais wa nchi hiyo, Kais Saied kuwa ni sawa ni kuhuisha tajiriba iliyofeli na kueleza kuwa, Tunisia inaelekea katika mkondo wa kurejea kwenye udikteta na kutengwa.
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Dec 30, 2021 11:36 UTC
  • Rached Ghannouchi
    Rached Ghannouchi

Rached Ghannouchi Spika wa Bunge lililosimamishwa la Tunisia amezitaja hatua na maamuzi yanayochukuliwa na Rais wa nchi hiyo, Kais Saied kuwa ni sawa ni kuhuisha tajiriba iliyofeli na kueleza kuwa, Tunisia inaelekea katika mkondo wa kurejea kwenye udikteta na kutengwa.

Al Ghannouchi ambaye pia ni mkuu wa chama cha Ennahdha amesisitiza kuwa, Rais Kais Saied anataka kuona Tunisia ikiwa nchi bila ya vyama vya siasa. Amesema: "Kinachoshuhudiwa sasa nchini Tunisia ni sauti moja ya Rais wa nchi na kwamba serikali inadhibitiwa na mtu mmoja ambaye anatekeleza chochote anachopenda. Yeye ndiye anayepasisha sheria na kufuta katiba, anafuta kazi Serikali na kulivunja Bunge ili aweze kudhibiti na kusimamia masuala yote ya nchi."  

Rais Kais Saeid wa Tunisia 

Tahadhari hii ya Rached Ghannouchi kwamba Tunisia inaelekea katika zama za udikteta ina mantiki kwa kuzingatia matukio ya karibuni nchini humo. Tunisia imekumbwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu Januari 25 mwaka huu. Rais Kais Saied wa nchi hiyo alichukua uamuzi wa ghafla na wa kushangaza wa kusitisha shughuli za Bunge na kuwafuta kazi Spika wa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, na kisha kuchukua udhibiti wa masuala yote ya nchi. Rais wa Tunisia alichukua maamuzi hayo kwa kisingizio kwamba, Waziri Mkuu wa nchi hiyo pamoja na serikali wameshindwa kuboresha hali ya uchumi na kukabiliana ipasavyo na maambukizi ya corona. Hatua hiyo ya Rais Kais Saied iliibua mivutano ya aina yake nchini Tunisia na tunaweza kuitaja mivutano hiyo kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu baada ya mapinduzi ya wananchi mwaka 2011 yaliyoiondoa madarakani serikali ya Bin Ali, rais wa wakati huo wa Tunisia. Harakati na hatua zote hizo za Rais Kais Saied ambazo zimejiri baada ya miezi kadhaa ya mivutano ya kisiasa zimekabiliwa na upinzani mkali wa ndani kutoka kwa wananchi na vyama vya siasa. Ali Laarayedh Naibu Mkuu wa chama cha Ennahdha ametangaza kuwa: "Maamuzi yaliyotangazwa na Rais ni mapinduzi dhidi ya taasisi za serikali, Katiba na mapinduzi ya wananchi wa Tunisia."  

Rais wa Tunisia aliyeng'olewa madarakani mwaka 2011  

Kais Saied katika miezi ya karibuni amechukua hatua mbalimbali za kuimarisha uwezo na mamlaka yake na kuwadhoofisha wapinzani. Hivi sasa kiongozi huyo wa Tunisia ana mpango wa kuifanyia marekebisho Katiba ambayo inagawanya madaraka ya kuongoza nchi kati ya Rais, Waziri Mkuu na Bunge. Rais wa Tunisia anaamini kuwa, mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo umesababishwa na Katiba iliyopasishwa mwaka 2014, na kwamba katiba hiyo haifai tena. Rais Kais Saied huko nyuma aliongeza muda wa kusitishwa shughuli za Bunge na kutangaza kuwa, kura ya maoni ya kitaifa kwa ajili ya kuifanyia marekebisho Katiba ya Tunisia itafanyika Januari 25  na uchaguzi wa Bunge tarehe 17 Disemba mwaka ujao wa 2022. 

Saied anasisitiza suala la kufanyiwa marekebisho Katiba katika hali ambayo, baadhi ya vyama vya siasa vikiwemo al Ennahdha, chama cha al Jumhuriya, Ettakatol, Afek Tounes, Amal na al-Tayyar al-Dimuqrati vinapinga mabadiliko ya aina yoyote ya Katiba. Vyama hivyo vimemtaka Rais Saied aheshimu ahadi zake kwa wananchi wa Tunisia na kufungamana na kiapo alichokula kabla ya kushika wadhifa wa Rais wa nchi. Vyama hivyo vya Tunisia pia vimelaani ukiukaji wa mara kwa mara wa haki na uhuru wa kimsingi ikiwemo haki za kusema na kuhukumiwa raia wa kawaida katika mahakama za kijeshi. Vilevile vimemtaja Rais Kais kuwa ndiye anayepasa kubeba dhima ya ukiukaji na ukandamizaji huo na vimetaka kusitishwa mara moja hatua hizo. 

Matukio yanayoshuhudiwa huko Tunisia na upinzani unaoshtadi wa wananchi na ule wa vyama vya kisiasa na pia indhari ya Rached Ghannouchi kiongozi wa chama cha Ennahdha, yote hayo yanaonyesha kuwa, mivutano ya ndani na ukosefu wa amani utaongezeka na kushadidi zaidi huko Tunisia iwapo Rais wa nchi hiyo ataendeleza hatua zake. Ni dhahir shahir kwamba, licha ya kupita miaka kumi tangu baada mapinduzi ya wananchi huko Tunisia mwaka 2011 si tu utulivu wa kisiasa uhaujarejea nchini humo bali demokrasia na matakwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ya wananchi yamekuwa ndoto isiyoabirika chini ya kivuli cha hitilafu zilizopo kuhusu suala la uongozi.

Maandamano ya wapinzani Tunisia dhidi ya Rais Kais Saied