Msambao wa Corona waongezeka Mauritania, rais pia aambukizwa
Rais Mohamed Ould Ghazouani wa Mauritania ameambukizwa ugonjwa wa Covid-19 huku maambukizi mapya ya maradhi hayo hatari yakiongezeka katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Serikali ya nchi hiyo imetangaza kuchukua hatua kadhaa za kudhibiti wimbi hilo jipya la maambukizo. Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo jana Ijumaa ilitoa dikrii ya kuwalazimisha wananchi kuvaa barakoa katika maeneo ya umma kama vile masokoni, kwenye migahawa na katika vyombo vya usafiri wa umma.
Kadhalika wizara hiyo imetangaza kuwa imetuma timu ya watu wa kufuatilia utekelezaji wa kanuni mpya zilizotangazwa kwa ajili ya kudhibiti msambao wa virusi hivyo.
Wakati huohuo, Kamati Maalumu ya Kutathmini Corona ya Mauritania imepiga marufuku mikusanyiko yote ya umma nchini humo, sambamba na kuagiza kufungwa kumbi zote za kuonesha filamu na michezo ya kuigiza. Kesi mpya 47,036 za ugonjwa wa Covid-19 ziliripotiwa jana nchini humo.
Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya Marais wa Botswana, Mokgweetsi Masisi na Filipe Nyusi wa Msumbiji kuambukizwa Corona.
Bara la Afrika limevuka visa milioni 10 vilivyorekodiwa vya maambukizi ya Covid-19, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likuonya juu ya tsunami kubwa na ya haraka ya maambukizo ya corona ambayo yanatatiza mifumo ya afya kote duniani.