Mlipuko wa kipindupindu umeua maelfu ya watu Nigeria
Mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu uliua maelfu ya watu nchini Nigeria katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.
Wizara ya Rasilimali za Maji ya Nigeria imesema jumla ya watu 3,598 waliaga dunia katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kutokana na ugonjwa wa kipindupindu mwaka jana wa 2021.
Emmanuel Awe, afisa wa wizara hiyo amesema kesi 107,911 za maradhi hayo ziliripotiwa mwaka jana katika majimbo 32 ya nchi hiyo.
Janga hilo la kipindupindu limeendelea kuchukua roho za watu nchini Nigeria katika hali ambayo, ni asilimia 14 tu ya wananchi wa nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 200 ndio wenye uwezo wa kupata maji safi na salama. Hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za serikali za mwaka juzi 2020.
Ugonjwa wa kipindupindu husababishwa na bakteria aina ya Vibrio Cholera na huenezwa kwa kunywa maji yasiyo salama. Dalili za ugonjwa huo ni maumivu ya tumbo, kuharisha, kutapika pamoja na homa.
Miripuko ya maradhi hayo hatarishi huripotiwa nchini Nigeria mara kwa mara, hususan katika misimu ya mvua za masika zinazoambatana na mafuriko.
Takwimu zinaonesha kuwa, watu bilioni 1.4 wapo katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa kipindupindu kote duniani, ambapo kwa wastani kesi milioni 2.8 za maradhi hayo huripotiwa kila mwaka, mbali na vifo zaidi ya 91,000.