DRC yawakamata wanaotuhumiwa kumuua balozi wa Italia
(last modified Thu, 20 Jan 2022 04:24:14 GMT )
Jan 20, 2022 04:24 UTC
  • DRC yawakamata wanaotuhumiwa kumuua balozi wa Italia

Vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimewatia nguvuni watu wawili wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa balozi wa Italia nchini humo.

Jenerali Abba Van, Kamishna wa Polisi katika mkoa wa Kivu Kaskazini amesema mbali na watuhumiwa wawili kutiwa mbaroni, lakini mshukiwa mkuu wa mauaji ya Luca Attanasio, aliyekuwa balozi wa Italia nchini humo angali anasakwa.

Amesema washukiwa wamehojiwa na kusema kuwa balozi huyo aliuawa katika tukio la utekaji nyara lililokwenda ndivyo sivyo, na kwamba watekaji waliitisha kikomboleo cha dola milioni moja.

Balozi huyo aliuawa mnamo Februari mwaka jana 2021, baada ya msafara wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP kushambuliwa ghafla mashariki mwa DRC.

Vyombo vya habari vya Kongo DR viliripoti kuwa, washambuliaji sita waliyaamuru magari katika msafara huo kusimama kwa kuweka vizuizi barabarani na kisha walifyatua risasi kiholela.

Mauaji ya balozi wa Italia nusra uvuruge uhusiano wa nchi hiyo na DRC

Hata hivyo kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, balozi Luca Attanasio na polisi mmoja wa Italia waliuawa katika hujuma iliyolenga msafara wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) katika eneo la Kanyamahoro karibu na mji wa Goma.

Hapo awali, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo alililaumu kundi la waasi wa nchi jirani ya Rwanda la FDLR kwa kuhusika na mauaji ya mwanadiplomasia huyo. Hata hivyo kundi hilo lilikanusha kuhusika na mauaji hayo na kudai kuwa wanajeshi wa Rwanda na DRC ndio waliohusika.