Simba waambukizwa Corona na wahudumu wa mbuga Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i79396-simba_waambukizwa_corona_na_wahudumu_wa_mbuga_afrika_kusini
Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini wamesema simba watatu na puma wawili waliopatikana na maambukizi ya virusi vya Corona waliambukizwa na wafanyakazi wa mbuga moja ya wanyamapori nchini humo.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jan 20, 2022 00:56 UTC
  • Simba waambukizwa Corona na wahudumu wa mbuga Afrika Kusini

Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini wamesema simba watatu na puma wawili waliopatikana na maambukizi ya virusi vya Corona waliambukizwa na wafanyakazi wa mbuga moja ya wanyamapori nchini humo.

Katika ripoti yao, wanasayansi hao wamesema simba na puma ambao wanatoka katika jamii ya paka wakubwa na ambao wamefungiwa sehemu kubwa, wapo katika hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 kutoka kwa wanadamu.

Utafiti wa wanasayansi hao umesema kuwa, wanyamapori hao wa mbuga moja ya binafsi mjini Johannesburg waliambukizwa virusi vya Corona mwaka jana na wahudumu ambao walikuwa wanawashughulikia.

Profesa Marietjie Venter, mhadhiri wa taaluma ya virusi katika Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini amesema, kirusi cha Corona kinachofahamika kitaalamu kama SARS-CoV-2 ambacho walipatikana nacho wahudumu wa mbuga hiyo, ndicho kilichopatikana kwenye sampuli za simba na puma hao.

Soko la samaki mjini Wuhan China, ambako ugonjwa wa Covid-19 unaripotiwa kuanzia

Wanasayansi hao wa Afrika Kusini waliamua kufanya utafiti huo baada ya kuona wanyama mwitu hao katika hifadhi hiyo ya kibinafsi wanasumbuliwa na matatizo ya kupumua, kutokwa na kamasi na kikohozi kikavu.

Utafiti huo umebainisha kuwa, wafanyakazi 12 wa mbuga hiyo walifanyiwa vipimo vya Corona, na matokeo yakaonyesha kuwa watano miongoni mwao walikuwa wameambukizwa; na hivyo kuna uwezekano mkubwa kuwa wao ndio waliambukiza wanyamapori hao.