Mahakama DRC yawahukumu kifo watu 51 kwa mauaji ya wataalamu wa UN
Mahakama ya kijeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imewahukumu kifo watu 51 kwa kupatikana na hatia ya kuhusika na mauaji ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa yaliyojiri katika mkoa wa Kasai nchini humo mwaka 2017.
Waendesha Mashitaka waliiomba mahakama ya Kananga iwahukumu kifo watuhumiwa 51 kati ya 54 waliofunguliwa mashitaka, ingawaje 22 miongoni mwao ni watoro, na kesi na hukumu dhidi yao zimetolewa pasi na wao kuwepo kortini.
Hukumu ya kifo huko DRC hutolewa tu mahakamani kwa maandishi, lakini kivitendo waliohukumiwa kifo hutumikia kifungo cha maisha jela, nchi ambayo ilifuta utekelezwaji wa hukumu wa kifo mwaka 2003.
Wataalamu hao wawili wa UN, Zaida Catalan, raia wa Sweden na Mmarekani Michael Sharp, ambao walikuwa wameitembelea Kasai kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha mgogoro katika eneo hilo la katikati mwa Kongo DR, walitekwa nyara tarehe 12 Machi mwaka 2017, na miili yao ilipatikana siku 16 baadaye.
Wataalamu hao waliouawa walikuwa sehemu ya timu ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ambao walitakiwa kufanya uchunguzi kuhusiana na upatikanaji wa zaidi ya makaburi 40 ya umati katika mkoa wa Kasai.
Eneo la Kasai la katikati mwa DRC limekuwa likishuhudia mapigano makali baina ya wanamgambo wa kikabila wa Kamwina Nsapu, kiongozi wa kundi la waasi wa eneo hilo na askari wa serikali tangu mwaka 2016.
Watu 3,400 waliripotiwa kuuawa, huku maelfu ya wengine wakilazimika kuwa wakimbizi katika mapigano hayo ambayo yalififia katikati ya mwaka 2017.