Uingereza yataka fukwe za Libya zizingirwe
Kamanda wa zamani wa jeshi la majini la Uingereza ametaka fukwe za Libya zizingirwe kila upande.
Televisheni ya Sky News imemnukuu Alan West akisema, kuna wajibu wa kuzingirwa kila upande fukwe za Libya kwa ajili ya kupambana na magendo ya wanadamu wanaoingia barani Ulaya.
Ameongeza kuwa, zoezi hilo linahitajia meli 10 za kivita, helikopta pamoja na ndege za kijasusi zisizo na rubani ambazo zina uwezo wa kukusanya taarifa na kusimamia usalama wa fukwe hizo.
Kamanda wa zamani wa Jeshi la Majini la Uingereza ameongeza kuwa, mpango wa David Cameron, Waziri Mkuu wa nchi hiyo wa kutuma meli moja ya kivita katika maji yanayoishia kwenye fukwe za Libya hautoshi na si chaguo bora.
Kamanda huyo wa zamani wa jeshi la majini la Uingereza amedai pia kuwa, kutumwa meli za kivita katika Bahari ya Mediterranean kwa ajili ya kuwaokoa wakimbizi wanaokaribia kuzama si fikra nzuri, kwani jambo hilo linazidisha ugumu wa kukabiliana na wimbi la wakimbizi hao.
Wiki iliyopita, Uingereza ilituma washauri wanne wa kijeshi katika kituo cha opereseheni maalumu za kupambana na magendo ya wanadamu cha Umoja wa Ulaya kilichoko nchini Italia.