May 28, 2016 16:02 UTC
  • Usalama warejea kikamilifu kaskazini mwa Uganda

Kamanda mmoja wa jeshi la Uganda amesema kuwa, hali ya usalama imesharejea kaskazini mwa nchi hiyo, na ndio maana sheria ya hali ya hatari imeondolewa.

Vyombo vya habari vimemnukuu Hasan Kato, mmoja wa makamanda wa kijeshi wa Uganda akisema kuwa, hali ya usalama imerejea katika mji wa Gulu, wa kaskazini mwa nchi hiyo, na hali ya hatari imeondolewa. Hali hiyo ya hatari iliwekwa baada ya watu wenye silaha kushambulia wanajeshi wa Uganda katika mji huo.

Hassan Kato ameongeza kuwa, hali ya usalama imerejea ingawa pia opereseheni za kukabiliana na makundi ya waasi bado hazijakatishwa.

Vile vile amewataka wananchi wa kaskazini mwa Uganda na hususan wa mjini Gulu kuwa watulivu na kushirikiana na vikosi vya serikali katika kudumisha amani na usalama kwenye eneo hilo.

Ikumbukwe kuwa eneo la kaskazini mwa Uganda liliwahi kuwa ngome kuu ya waasi wa Kikristo wa LRA wanaopigania kusimamisha utawala wa sheria 10 za Biblia.

Mwaka 2005, Mahakama ya Jinai ya Kimataifa ICC ilitoa amri ya kukamatwa kiongozi wa waasi hao Joseph Kony na viongozi wengine waandamizi wa genge hilo kwa tuhuma za kufanya jinai nyingi za kivita.

Tags