Sheikh Zakzaky awataka walimwengu wakabiliane na mashambulio ya Saudia dhidi ya Yemern
Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amewataka walimwengu kujitokeza na kukabiliana na hujuma na mashambulio ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya wananchi madhulumu wa Yemen.
Sheikh Ibrahim Zakzaky amesema kuwa, kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya jinai na mashambulio ya utawala vamizi wa Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen hakina maana.
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema hayo katika mkutano uliofanyika kwa njia ya mawasiliano intaneti uliokuwa ukijadili wigo wa hujuma na mashambulio dhidi ya Yemen na kubainisha kwamba, mashambukio hayo ni jinai za kivita dhidi ya jamii ya mwanadamu.
Sheikh Zakzaky amesisitiza kuwa, njia pekee ya kukabiliana na mashambulio ya muungano vamizi wa Saudia dhidi ya Yemen ni muqawama na kusimama kidete na kwamba, ana matumaini wananchi wa Yemen wataibuka na ushindi na kuviangamiza haraka iwezekanavyo vikosi vya mabeberu.
Kadhalika kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ameashiria jinai zilizotokea katika nchi za Libya, Iraq na Syria na kubainisha kwamba, jinai hizo zinashabihiana na zinazofanyika hivi sasa nchini Yemen.
Saudi Arabia huku ikiungwa mkono kwa hali na mali na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Marekani, utawala wa Kizayuni, Uingereza na nchi kadhaa nyingine mwezi kama vile Sudan, mwezi Machi mwaka 2015 ilianzisha mashambulizi ya kijeshi ya pande zote dhidi ya Yemen na kuiwekea mzingiro wa angani, baharini na nchi kavu nchi hiyo maskini ya Kiarabu.
Hadi sasa Wayemeni zaidi ya elfu 16 wameshauawa katika vita hivyo vya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia, huku makumi ya maelfu ya wakijeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.