Nchi za Ulaya zaendelea kuondoa wanajeshi wao 'vamizi' Mali
Waziri wa Ulinzi wa Estonia amesema nchi hiyo ya kaskazini mwa Ulaya imekata shauri ya kuwaondoa wanajeshi wake nchini Mali, na hivyo kuwa nchi ya hivi punde zaidi ya Ulaya kuchukua hatua hiyo baada ya Denmark.
Kalle Laanet, Waziri wa Ulinzi wa Estonia amesema uwepo wa Vikosi vya Ulinzi vya Estonia (EDF) nchini Mali unaelekea kufika ukingoni, na tangazo kuhusu uamuzi huo litatolewa rasmi leo Jumatano.
Haya yanajiri wiki chache baada ya Denmark kuanza kuondoa wanajeshi wake katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, ambao walitumwa nchini humo kama sehemu ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Ufaransa, baada ya kutakiwa kufanya hivyo na serikali ya Bamako.
Hapo jana pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian alisema wanajeshi wa nchi hiyo wataendelea kupambana na kile alichokitaja kuwa 'ugaidi' katika eneo la Sahel na si nchini Mali.

Wanajeshi wa nchi hizo za Ulaya katika eneo la Sahel barani Afrika wanahudumu katika oparesheni Barkhane na ni sehemu ya kikosi kazi cha kimataifa cha Takuba, licha ya wananchi wa nchi za kanda hiyo ya magharibi mwa Afrika kuandamana mara kadhaa wakishinikiza kuondoka vikosi hivyo vamizi.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Mali, Choguel Kokalla Maiga, aliishutumu serikali ya kikoloni ya Ufaransa kwa vitendo vyake dhidi ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi na kusema kuwa, Wafaransa walipaswa kuisaidia Mali, lakini badala yake wanayasaidia magenge ya kigaidi yanayopigania kujitenga na wanazichochea nchi za Ulaya ziliwekee vikwazo taifa hilo la Kiafrika.