Watu 15 wauawa katika shambulio la wabeba silaha DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i80398-watu_15_wauawa_katika_shambulio_la_wabeba_silaha_drc
Kwa akali watu 15 wameuawa katika shambulio la kundi moja la wabeba silaha katika mkoa wa Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Feb 15, 2022 23:11 UTC
  • Watu 15 wauawa katika shambulio la wabeba silaha DRC

Kwa akali watu 15 wameuawa katika shambulio la kundi moja la wabeba silaha katika mkoa wa Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Chifu wa kijiji cha Syeri Aberkozo,  Innocent Matukadala ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, wapiganaji hao walivamia kijiji hicho na kuanza kuwashambulia wakazi wake kwa mapanga.

Matukadala ameeleza kuwa, mbali na watu 15 kuuawa, wengine wanne wamejeruhiwa, huku majeruhi wawili wakiwa katika hali mahututi.

Chifu huyo amesema kundi la wanamgambo wa CODECO ndilo lililohusika na hujuma hiyo ya Jumanne dhidi ya wakazi wa kijiji cha Syeri Aberkozo.

Naye Maki Kilota Gale, mkulima katika kijiji kinachopakana na Syeri Aberkozo ambaye alipigwa risasi mguuni akikimba shambulio hilo la waasi wa CODECO, amepoteza jamaa zake kadhaa katika hujuma hiyo.

Askari wa DRC wakilinda doria

Amesema hafahamu ni kwa nini wanamgambo hao wanatekeleza hujuma hizo za mara kwa mara dhidi ya wanavijiji wasio na hatia mkoani Ituri.

Mapema mwezi huu, wanamgambo hao wa CODECO walilenga kambi ya wakimbizi wa ndani ya Savo katika shambulio la kutisha katika mkoa wa Ituri, na kuua watu 60.