Magaidi 20 wa al-Shabaab waangamizwa na askari wa AMISOM, Somalia
Wanachama zaidi ya 20 wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni ya askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM).
Duru za kiusalama zinaarifu kuwa, wanajeshi wa AMISOM walishambulia maficho ya al-Shabaab katika jimbo la Lower Shabelle na kuua 20 miongoni mwao, baada ya magaidi hao kufanya hujuma ya umwagaji damu katika mji mkuu Mogadishu, na kuteka kwa muda kituo cha polisi cha wilaya ya Kahda.
Habari zaidi zinasema kuwa, askari wa AMISOM wameshirikiana na wanajeshi wa serikali ya federali ya Somalia katika operesheni hiyo dhidi ya wanachama wa kundi hilo la kitakfiri.
Juzi Jumatano, watu sita waliuawa huku wengine wasiopungua 16 wakijeruhiwa baada ya wanachama wa al-Shabaab kushambulia vituo vya polisi na vya upekuzi katika mji mkuu Mogadishu.
Kundi la kigaidi la al Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida mara kwa mara limekuwa kilifanya hujuma na kutekeleza mashambulizi dhidi ya maeneo ya serikali na wiki iliyopita kundi hilo lililishambulia basi lililokuwa limewabeba makamisha wa uchaguzi.
Kundi hilo la kigaidi limefanya hujuma hiyo huku Somalia ikijiandaa kwa uchaguzi wa rais ulioakhirishwa mara kadhaa.