Wahajiri 700 wafa maji pwani ya Libya wakielekea Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8050-wahajiri_700_wafa_maji_pwani_ya_libya_wakielekea_ulaya
Mamia ya wahajiri wamepoteza maisha baada ya boti zao kuzama katika pwani ya Libya katika muda wa siku chache zilizopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 29, 2016 09:34 UTC
  • Wahajiri 700 wafa maji pwani ya Libya wakielekea Ulaya

Mamia ya wahajiri wamepoteza maisha baada ya boti zao kuzama katika pwani ya Libya katika muda wa siku chache zilizopita.

Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema kuwa, yumkini watu 700 wameaga dunia baada ya boti zao kuzama katika pwani ya Libya, kusini mwa Italia, kati ya Jumatano na Ijumaa iliyopita.

Taarifa ya UNHCR imeongeza kuwa, wahamiaji hao walizama kwa kutumia vyombo vya usafiri visivyoweza kumudu mawimbi ya bahari wakiwa katika juhudi za kuingia barani Ulaya. Habari zinasema kuwa, watu 100 wanahofiwa kupoteza maisha baada ya boti yao kuzama siku ya Jumatano, huku wengine 550 wakizama baada ya boti yao kuzama karibu na bandari ya Sabratha, katika pwani ya Libya siku ya Alkhamisi. Habari zaidi zinasema kuwa, watu 45 waliaga dunia baada ya boti yao kuzama kusini mwa Italia huku 135 wakiokolewa siku ya Ijumaa.

Haya yanajiri siku chache baada ya Uingereza kutangaza kuwa itatuma meli ya kivita nchini Libya kuzuia wahamiaji wa kigeni ambao wanatumia pwani ya nchi hiyo kuvuka Bahari ya Mediterranean na kuingia Ulaya kinyume cha sheria, aghalabu yao wakitokea nchi za Kiafika kama Somalia, Sudan, Ethiopia na Misri . Wakimbizi karibu laki mbili wameingia Ulaya kupitia bahari ya Mediterranean katika mwaka huu pekee huku mamia ya wengine wakifariki dunia kwa kuzama baharini.