Watu 14 wauawa baada ya gaidi kujiripua kwa bomu Somalia
Kwa akali watu 14 wamepoteza maisha baada ya gaidi aliyekuwa amejifunga bomu kujiripua katika eneo lenye shughuli nyingi katikati mwa Somalia.
Abdirmahad Hussein, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, gaidi huyo alijiripua ndani ya mgahawa mmoja katika mji wa Beledweyne, makao makuu ya eneo la Hiran la katikati mwa Somalia.
Televisheni ya Taifa ya Somalia imetangaza kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, watu 14 wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi la jana Jumamosi.
Kundi la kigaidi la al Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida ambalo mara kwa mara limekuwa kilifanya hujuma za namna hii za kutekeleza mashambulizi dhidi ya maeneo ya serikali na raia, limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ya jana.
Haya yanajiri siku chache baada ya wanachama zaidi ya 20 wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab kuangamizwa katika operesheni ya askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) katika jimbo la Lower Shabelle.
Operesheni hiyo ya AMISOM ilikuwa ya ulipizaji kisasi baada ya magaidi hao kufanya hujuma ya umwagaji damu katika mji mkuu Mogadishu, na kuteka kwa muda kituo cha polisi cha wilaya ya Kahda.
Jumatano iliyopita, watu sita waliuawa huku wengine wasiopungua 16 wakijeruhiwa baada ya wanachama wa al-Shabaab kushambulia vituo vya polisi na vya upekuzi katika mji mkuu Mogadishu.