Jeshi la Niger laangamiza wanachama 12 wa Boko Haram
(last modified Sun, 29 May 2016 14:17:47 GMT )
May 29, 2016 14:17 UTC
  • Jeshi la Niger laangamiza wanachama 12 wa Boko Haram

Jeshi la Niger limetangaza kuwa limeangamiza wanachama 12 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika kijiji cha Bosso, kusini mashariki mwa eneo la Diffa karibu na mpaka na Nigeria.

Kanali Moustapha Ledru, msemaji wa jeshi la Niger amesema wanamgambo hao wameagamizwa katika makabiliano makali na jeshi la nchi hiyo katika eneo la Bosso, ambalo limeshuhudia mashambulizi ya magaidi hao katika kipindi cha wiki moja iliyopita. Amesema jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kunasa silaha kadhaa za genge hilo la kigaidi, zikiwemo bunduki, maroketi na simu za rununu.

Kwa mujibu wa Ibrahim Chetima, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, makabiliano hayo yalidumu kwa muda wa masaa 15 ambapo wanakijiji hao walilazimika kujificha katika eneo la misitu linalopakana na eneo la Borno.

Kundi la Boko Haram lililoanzisha machafuko ya ndani nchini Nigeria mwaka 2009 limeua zaidi ya watu elfu 20 na kulazimisha mamilioni ya wengine kukimbia maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo. Kundi hilo pia limepanua mashambulizi yake ya kigaidi katika nchi jirani kama Cameroon, Chad na Niger. Licha ya nchi kadhaa za Kiafrika kuungana kwa ajili ya kupambana na kundi la Boko Haram, lakini hadi sasa zimeshindwa kuwatokomeza wanamgambo hao.

Tags