Mahakama Tanzania yamuachia huru Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81016-mahakama_tanzania_yamuachia_huru_mwenyekiti_wa_chadema_freeman_mbowe
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Freeman Mbowe na wenzake watatu, leo Ijumaa wamefutiwa mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 04, 2022 12:24 UTC
  • Mahakama Tanzania yamuachia huru Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Freeman Mbowe na wenzake watatu, leo Ijumaa wamefutiwa mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Mbowe na wenzake wameachiwa baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, DPP, kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo.

Wakili wa Serikali, Robert Kidando amesema, Mkurugenzi Wa Mashitaka (DPP) kwa niaba ya Jamhuri anaomba kuwasilisha taarifa ya kutokuwa na nia na kuendelea na shauri hili kwa njia ya maandishi.

Amesema: Taarifa hiyo tunaitoa chini ya Kifungu cha 91(1) kwa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Mheshimiwa Jaji kwa maombi hayo ya kifungu cha 91(1) tunaomba kuondoa mashitaka yote dhidi ya washitakiwa wote.

Taasisi, mashirika na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania wamekuwa wakitoa mwito na kushinikiza kiongozi huyo wa upinzani nchini Tanzania aachiwe huru.

Mbowe mahakamani

Kiongozi huyo wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, alitiwa mbaroni alfajiri ya kuamkia Julai 21 mwaka jana 2021, akiwa katika hoteli moja katika mtaa wa Ghana alikokifikia kwa ajili ya kushiriki kongamano la Katiba Mpya lililoandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha).

Siku iliyofuata Jeshi la Polisi nchini humo liliueleza umma kuwa Mbowe anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo za kupanga njama za kufanya vitendo vya kigaidi na kuua viongozi wa Serikali.