Watu 27 wauawa katika shambulio la waasi wa ADF nchini DRC
Watu wasiopungua 27 wameuawa huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, katika shambulio jipya la wanamgambo wa Uganda wa ADF.
Duru za habari zinaarifu kuwa, wapiganaji wanaosadikika kuwa wa ADF usiku wa kuamkia jana Jumamosi walishambulia kijiji cha Mamove katika eneo la Beni, mpakani mwa mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri na kufanya mauaji hayo ya kikatili.
Kinos Katuho, kiongozi wa shirika la kijamii la Mamove amesema raia hao waliuawa kwa kupigwa mapanga wakiwa ndani ya majumba yao na wengine walikuwa katika viwanja vyao.
Katuho ameeleza kuwa, "baadhi ya watu hawajulikani walipo kufuatia shambulio hilo, huku makumi ya nyumba zikichomwa moto. Idadi kubwa ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao na kutorokea katika maeneo tofauti."
Habari zaidi zinasema kuwa, makumi ya miili ya wahanga wa unyama huo imepelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Oicha, huku mingine ikisalia katika eneo la tukio.
Mwisho mwa Januari mwaka huu, raia wengine 12 waliuawa katika mkoa wa Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kufuatia mashambulio ya waasi hao wa ADF.
Kundi hilo la waasi linalotokea kaskazini mashariki mwa Uganda limekuwa likiendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa DRC tangu muongo wa 90, ambapo limeua mamia ya watu, na kupelekea malaki ya wengine kuwa wakimbizi.